Mikoa minne ya Tanzania kukumbwa na mvua kubwa

     
Mara nyingi panapokuwepo na mvua kubwa huleta athari kwa watu na mali (Picha na mtandao)
Zikiwa zimebaki siku chache kuumaliza mwaka 2017 mamlaka  ya Hali ya Hewa Tanzania imesema kuelekea  mwisho wa mwaka huu  mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha katika mikoa minne ya Tanzania  ambayo ni  Rukwa Mbeya, Songwe na Kigoma.
   Hayo yamesemwa na Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa Hali ya Hewa  Bwana Samuel Mbuya na kueleza kuwa  mikoa hiyo minne ndio inatarajiwa kuwa na mvua wakati huu wa mwisho wa mwaka  na kwa mikoa mingine ya Pwani na Dar es salaam ifikapo mwisho wa mwezi huu, mvua za vuli zinazoendelea kunyesha mikoa hiyo  zitakuwa zimefikia ukingoni.
      Meneja huyo amesema kuwa mamlaka ya hali ya hewa inatarajia mvua zitaendelea kunyesha katika maeneo ya mikoa ya Magharibi ambayo ni Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Lindi, Dodoma na Singida ambazo  zilianza kunyesha Novemba  zinatarajiwa kumalizika Aprili.
        Mbuya amesema maeneo mengine katika mikoa ya Tanzania  kutakuwa na mvua za kawaida huku mikoa minne ikiwa na mvua kubwa.
         Aidha bwana Mbuya  amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa  mara kwa mara ili wapate  mwelekeo wa hali ya hewa na tahadhari wanazotakiwa kuchukua.

No comments:

Post a Comment